Viongozi wasichana vyuoni- Sehemu ya 1

 Tarehe 30 na 31 Aprili, nilifanikiwa kushiriki mkutano wa viongozi wanavyuo ulioendeshwa na jukwaa la wafeminia vijana (Young Feminist Forum) chini ya Tanzania Gender Networking Programme (TGNP), uliokuwa unalenga kuwakutanisha wasichana viongozi vyuoni kujadili masuala mbalimbali yahusuyo ufeminia na jinsia.

YFF Ni jukwaa la vijana wafeminia, TGNP iligundua umuhimu wa vijana katika kusogeza gurudumu la usawa wa kijinsia kwenye jamii. Ili kuwakutanisha, walionao vyema kuanzisha jukwaa hili, ili kuruhusu vijana kukutana kujadili changamoto na kutafuta njia bora zaidi ya kuzitatua.

Mojawapo ya sehemu zilizovutia zaidi washiriki katika mkutano huu, Ni namna viongozi wasichana walivyoeleza uzoefu wao kwenye masuala ya uongozi. Wasichana walipata kujifunza kupitia uzoefu wao wenyewe na kupeana changamoto katika nafasi zao.

Hii Ni sehemu ya kwanza, ikiwa imebeba hadithi ya msichana kwenye safari yake ya uongozi.

..........


Anaitwa Zubeda Kaduguda, msichana mwenye umri wa miaka 23. Kwa sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo cha usimamizi wa fedha “Institute of Finance and Management” IFM- Dar es salaam, akichukua shahada ya uhasibu. 

Alianza safari yake ya uongozi akiwa na umri mdogo, amefanikiwa kushika nafasi kadha wa kadha akiwa shule ya msingi na sekondari kama dada mkuu na kiranja wa nidhamu. 

“Nilikuwa najiona ni kiongozi, na niliwajibika sehemu yangu kwa nafasi hizo” anasema Zubeda.

Zubeda anaamini katika kutokukata tamaa, na kupigania unachokipenda. Nguvu hii ilimvuta zaidi kutimiza sehemu ya ndoto zake katika Nyanja ya uongozi.

Baada ya kufika chuo, Zubeda alijihusisha na masuala ya uongozi na akafanikiwa kuwa mmojawapo wa wagombea wa nafasi ya uraisi. Kuwa msichana peke yake, kulimfungua akili zaidi namna ambavyo wasichana hawashiki nafasi hizo za juu za uongozi, sio tu serikalini, bali hata vyuoni.

Alifanikiwa kushinda kiti cha uraisi, na  kwa sasa Zubeda ni Raisi wa kwanza msichana wa serikali ya wanafunzi wa chuo cha usimamizi wa fedha, IFM. 

Zubeda anagusia baadhi ya mambo anayoshuku yamevuta zaidi kwenye nafasi kubwa za uongozi kama hizi, ni pamoja na, kujihimiza mwenyewe, kuwa na nidhamu, kujishusha kwa anaowatumikia na kuwajibika kwa nafasi yake. Aligusia pia suala la ubinadamu na kujihisi vile wengine wanajihisi, “kuvaa viatu vyao kipindi wanapoguswa na changamoto”.

Suala la uongozi kwa Zubeda, ni jambo analolipenda na anafanya kwa upendo. Zubeda anasema, “Nafurahia kuongoza, na kutimiza majukumu yangu ya uongozi ni kitu ninachopenda zaidi, kwa sababu, ninagusa maisha ya watu moja kwa moja”.

Mbali na mafanikio yake, kama watu wengine, Zubeda anapitia changamoto mbalimbali kwenye uongozi wake, haswa kama kiongozi msichana. Changamoto hizo ni kama, mawazo hasi kuhusu yeye kama mwanamke kushika nafasi hiyo ya uongozi. 

Yeye anaendelea kujiamini na akiamini zaidi changamoto ni sehemu ya ukuaji wake katika safari yake ya uongozi.

Mwisho, Zubeda anagusia kwamba, asilimia 80% ya ahadi alizoahidi wakati wa kugombeas uraisi wa chuo, ameshatimiza, na anayopendezwa nayo zaidi ni kuanzisha dawati la jinsia chuoni, ambalo linasaidia wanachuo haswa wasichana kupatiwa usaidizi wanapokumbwa na changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya jinsia. Wasichana wako huru kufikisha changamoto zao, na hufarijika zaidi wanapomkuta msichana mwenzao, Zubeda, akiwashika mkono kuzitatua. 

Moja ya ndoto za Zubeda ni kufanya kazi katika mashirika makubwa ya kimataifa ili aendelee kugusa maisha ya watu bila kuzingatia rangi, dini, kabila, jinsia ama hali ya kiuchumi.

Hakika, Zubeda ni mfano mzuri wa kuigwa, na tunaiona safari yake ya uongozi kufika juu zaidi ili aendelee kugusa maisha ya watu wengi zaidi.

Post a Comment

1 Comments

Emoji
(y)
:)
:(
hihi
:-)
:D
=D
:-d
;(
;-(
@-)
:P
:o
:>)
(o)
:p
(p)
:-s
(m)
8-)
:-t
:-b
b-(
:-#
=p~
x-)
(k)